WIMBO WA NGAZI

Wimbo wa ngazi

Kila jinsia na rika 
Makabila ya watu
Tulizunguka kijijini
Kwa lengo na sauti moja
Nyuso zilitumwekamweka kwa furaha 
Wanyonge tulichangamka na kukaramka

Vipofu
Viziwi 
Na viwete 
Tukakusanyika kwa pamoja kama nyuki
Ili tuifanikishe siku yako 
Ajabu! 
Asubuhi saa kumi ukiwa unakorota 
Tayari tulikuwa foleni 
Watoto wachanga wakitulilia migongoni 
Tukakukabidhi ngazi kwa furaha
Upande juu ya mbuyu kwa furaha
Upupue majani tupate
Upukuse matawi tupate matunda
Wanyonge tukawa na imani ya kupunguza
Mateke ya njaa na makofi ya jua hapa chini ya jua
Ukapanda ukafika
Tukakungoja 
Tukaanza kusoma sura yako
Na maneno mateule gazetini 
Sauti yako tukawa tunaisikia redioni
Tunakungojea 
Ajabu! 
Ulipofika kitu cha kwanza
“Yuko wapi mke wangu, barafu itanigandisha” 
Tukakupatia
“Kizao changu je?” 
Tukakupatia
Mkashirikiana 
Kujenga mnara wa Babeli
Orofa za kiajabu
Mkanunua ndege za kutembea angani
Nje tukaona kitambaa chetu chenye rangi ya uhuru 
Juu ya nguzo ndefu 
Mkatabasamu  mmefika 
Ajabu! 
Wewe, mke na uzao wako mkalewa utamu
Utamu wa hewa na mazingira ya aina yake
Utamu wa sauti tamu na henezi za nyuni 
Wanaoghani mashairi ya kuongoaongoa
Mkalewa kabisa… 
Ukaiba, uachi kuiba, chochote hapa chini
Ukabeba, yote akraba, kaiweka mbuyuni
Sasa leba, kawa kinasaba, ya vimondo kitwani
Mchunge mali yenu, tusiibe!
Chini ya mbuyu tulipiga magoti
Machozi yakitudondoka njia nne nne
Aliyekuwa analiliwa hakuwa na habari
Tulilia …
Watoto wetu hawana karo
Mashamba yetu yananyakuliwa
Barabara ulizoacha ni mbovu hazipitiki
Tunarudije makwetu?
Mamluki wanatutishia maisha
Hatuna stima, moshi wa kibatari
Unahatarisha afya zetu
Mateke ya njaa
Makofi ya jua
Makonde ya mafuriko
Tunaangamia
Ajabu! 
Maji yako ya kunywa  nembo  
Ni ya  Made in Wuhan ng’ambo
Chakula ni cha ng’ambo
Watoto wako shuleni ng’ambo
Mke wako ajifungulia ng’ambo
Majina ya watoto wenu ni ya ng’ambo
Tena hawajui kiswahili, lugha yenu kimombo
Lugha ya mama imeghafilika
Nyaka tano ikianza kuinama
Tunakuona 
Unatoka kwa mabawa
Unaingia kwa magurudumu
Tena unakanyaga kwa maringo
Ulinzi ni wa nyuki 
Ndege juu
Pikipiki kando
Vifaru mbele
Nyuma, ajabu
Wasanii walevi tena watupu hawafichi vya sirini
Wapo tu juu ya makarandinga
Wakiimba  nyia 
(Nitunzie ngazi uyaone maajabu)x2
(Barabara nitajenga ujangili utaisha, stima mtapata bure Nani kama mimi) x2
chorus
Nyeka oyeeeeeeeeeeeeee!
(Ni nani ataikomboa ngazi) x2
(Ni nani)x4 ataikomboa ngazi… 
Unaturushia matunda mawili 
Watu elfu mbili
Tunang’ang’ania 
Tunakanyagana
Tunauana
Ajabu! 
Sasa, 
Maradhi yamefika kutoka ng’ambo kimya
Maji ya kunywa  ni ya kisima  kimya
Shule zimefungwa mke ni mjamzito unatafuta mkunga kimya
Uwanja wa ndege umefungwa utaendaje ng’ambo? kimya 
Hela ulonazo? Ndio ! Kimya
Ombi langu ni uradhike 
Ushuke chini kwa tusi futi sita
Umwombe msamaha 
Ken Walibora kimya
Ajabu!
Painkiller Malenga Sera

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *